بسم الله الرحمن الرحيم

kutafuta elimu ni faradhi kwa kila muislamu
الحمد لله الذي نستعينه ونستغفره ونعوذ بالله من شرور أنفسنا ومن سيئات أعمالنا من يهد الله فلا مضل له ومن يضلل فلا هادي له .



ونشهد أن لا إله إلا الله وحده لا شريك له ونشهد أن محمدا عبده ورسوله أرسله بالهدى ودين الحق ليظهره على الدين كله وكفى بالله شهيدا




TUKIO LA ISRAA NA MIIRAJI

Tukio La Israa Na Mi’raaj

بسم الله الرحمن الرحيم

Kutokana na umuhimu wa tukio hili ambalo Allaah سبحانه وتعالى Kalielezea katika Kitabu Chake Kitukufu pale Anaposema:


((سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَى بِعَبْدِهِ لَيْلاً مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ إِلَى الْمَسْجِدِ الأَقْصَى الَّذِي بَارَكْنَا حَوْلَهُ لِنُرِيَهُ مِنْ آيَاتِنَا إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ البَصِيرُ))


((Ametakasika Aliyemchukua mja Wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyouzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara Zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona)) [Al-Israa: 1]


Na ni Mu’ujizah mkubwa kabisa wa Nabii yetu kipenzi صلى الله عليه وآله وسلم baada ya Mu’ujizah wa Qur-aan Tukufu, kuna haja ya kukieleza tena japo kimekwishaelezwa na kuandikwa na wengi.

Tukio hili adhimu, limeelezwa na wanahistoria kwa kauli mbalimbali wakati hasa lilipotukia:


1. Inasemekana Israa ilikuwa katika ule mwaka ambao Allaah سبحانه وتعالى Alimkirimu ndani yake Utume, Ameichagua kauli hii Atw-Twabariy.


2. Inasemekana Israa ilikuwa baada ya kupewa Utume kwa miaka mitano, Kauli hii imepewa nguvu na Al-Nawawiy na Al-Qurtwubiy.


3. Inasemekana Israa ilikuwa usiku wa ishirini na saba katika mwezi wa Rajab, Mwaka wa kumi wa Utume, Kauli hii imepewa nguvu na mwanachuoni mkubwa Al-Mansuur Forty.


4. Inasemekana Israa ilikuwa kabla ya Hijra kwa miezi kumi na sita yaani katika mwezi wa Ramadhaan mnamo mwaka wa kumi na mbili wa Utume.


5. Inasemekana Israa ilikuwa kabla ya Hijra kwa mwaka mmoja na miezi miwili yaani Muharram mnamo mwaka wa kumi na tatu wa Utume.


6. Inasemekana Israa ilikuwa kabla ya Hijra kwa mwaka mmoja yaani Rabi’u Ath-Thaaniy mnamo mwaka wa kumi na tatu wa Utume.


Kauli tatu za mwanzo zimepingwa kwa sababu Mama wa Waumini Khadiyjah رضي الله عنها alifariki mwezi wa Ramadhaan mwaka wa kumi wa Utume na kifo chake kilitokea kabla ya kufaradhishwa kwa Swalaah tano na hakuna tofauti kuwa Swalaah tano zilifaridhishwa katika usiku wa Israa. Ama kuhusu kauli tatu zilizobaki hakikupatikana kile ambacho kingetumika kutia nguvu moja katika kauli hizo isipokuwa mtiririko wa Surat Al-Israa, Ambao unafahamisha kuwa Israa ilichelewa sana. Wanachuoni wa Hadiyth wamepokea ufafanuzi wa tukio hili na hapa chini tunauleta kwa ufupi katika maneno yafuatayo:


Ibn Al-Qayyim amesema; “Mjumbe wa Allaah صلى الله عليه وآله وسلم, kwa kauli sahihi, alipelekwa kimwili akiwa amempanda Buraaq, akifuatana na Jibriyl عليه السلام kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Baytul Al-Maqdis, akamfunga Buraaq katika kikuku cha mlango wa Msikiti, Na kisha kuswali pamoja na Mitume, Yeye akiwa Imaam. Baada ya hapo, usiku huo huo kutoka Baytul Al-Maqdis akapandishwa katika uwingu wa Dunia akifuatana na Jibriyl عليه السلام aliyekuwa akibisha hodi kwa ajili yake, akafunguliwa na huko akamuona Aadam عليه السلام baba wa watu wote, akamsalimia, akamkaribisha na akamjibu salaam yake na akaukubali Utume wake. Allaah سبحانه وتعالى Akamuonyesha roho za watu wema zikiwa upande wake wa kuume na roho za watu waovu zikiwa upande wake wa kushoto. Baada ya hapo akapandishwa uwingu wa pili, Jibriyl عليه السلام akaomba kuingia, akafunguliwa na hapo akamuona Yahya bin Zakariya na ‘Iysa bin Maryam عليهما السلام, akakutana nao, akawasalimia, na wao wakamjibu salaam yake, Wakamkaribisha na kisha wakaukubali Utume wake. Kisha akapandishwa mpaka uwingu wa tatu, hapo akamuona Yuusuf عليه السلام, akamsalimia, naye akamjibu salaam yake, akamkaribisha na akaukubali Utume wake. Baada ya hapo akapandishwa uwingu wa nne ambako alimkuta Idriys عليه السلام, akamsalimia, naye akamjibu salaam yake, akamkaribisha na akaukubali Utume wake. Kisha akapandishwa uwingu wa tano, Na hapo akamuona Haaruun bin ‘Imraan عليه السلام, akamsalimia, naye akajibu salaam yake na kumkaribisha na kuukubali Utume wake.

Baada ya hapo akapandishwa katika uwingu wa sita na akamkuta hapo Muusa bin Imraan عليه السلام, akamsalimia, naye akajibu salaam yake, akamkaribisha na akaukubali Utume wake. Alipompita, Muusa عليه السلام alilia na alipoulizwa ni jambo gani linalimliza? Akajibu, “Ninalia kwa sababu kijana amepewa Utume baada yangu, Na katika Ummah wake wataingia peponi kuliko watakaoingia peponi kutoka katika Ummah wangu.” Kisha akapandishwa kwenye uwingu wa saba, ambako alikutana na Ibrahiym عليه السلام, akamsalimia naye akajibu salaam yake, akamkaribisha na akaukubali Utume wake. Baada ya hapo ndipo akanyanyuliwa na kupelekwa Sidratul-Muntahaa, Kisha akanyanyuliwa hadi Baytul Ma’amuur, naye akapandishwa kupelekwa kwa Allaah Mwingi wa Utukufu, Akasogea Mtume صلى الله عليه وآله وسلم mpaka umbali wa kiasi cha masafa ya Qawsayn (pinde mbili) au karibu zaidi kuliko hivyo, Allaah سبحانه وتعالى Akayafunua kwa Mja wake yale Aliyoyafunua, Na Akamfaradhishia Swalaah Khamsini. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم Akazipokea na kuanza kurejea mpaka alipofika mahali alipo Muusa عليه السلام ambaye alimuuliza; “Umepewa amri ya jambo gani? Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akamueleza, “Ameniamrisha Swalaah Khamsini”, Muusa عليه السلام akamwambia, “Kwa hakika Ummah wako hawataweza kutekeleza jambo hilo, Rejea kwa Mola wako na umuombe Akupunguzie iwe takhfifu kwa Ummah wako”. Akageuza uso na kumuangalia Jibriyl عليه السلام kwa jicho la kumtaka ushauri katika jambo hilo, naye akampa ishara ndio kama ukitaka. Akapanda naye Jibriyl عليه السلام mpaka akafika kwa Allaah سبحانه وتعالى na hali ya kuwa Yeye Yu Mahali Pake; (Tamko hili ni la Al-Bukhaariy). Katika mapokezi mengine, Akampunguzia Swalaah kumi kisha akateremshwa mpaka mahali alipokuwa Muusa عليه السلام na akamueleza idadi ya Swalaah zilizopunguzwa. Muusa عليه السلام akamwambia, “Rejea kwa Mola wako na umuombe Akupunguzie tena. “Inasemekana kuwa hakuacha kwenda na kurudi kwa Muusa عليه السلام na Allaah سبحانه وتعالى mpaka Swalaah zikabaki tano. Muusa عليه السلام akamtaka arejee kwa Allaah tena na kuomba kupunguziwa, Hapo Mtume akajibu; “Kwa hakika ninamuonea hayaa Mola wangu na sasa mimi ninaridhia na ninakubali Swalaah nilizopewa.” Alipokwenda umbali kidogo, Alilingania mlinganiaji; “Nimezipitisha faradhi Zangu na nimewapunguzia waja Wangu.”


Ibnul Qayyim amejadili kuhusu suala hili la Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kumuona Mola wake, Allaah Aliyetukuka mwenye Utukufu na kisha akayataja maneno ya Ibn Taymiyah kuhusu suala hili. Matokeo ya utafiti ni kuwa, “Kumuona Allaah سبحانه وتعالى kwa macho ni jambo ambalo halikuthibiti kabisa. Hiyo ni kauli ambayo haikusemwa na yeyote katika Maswahaba. Na kile tunachokisema kutoka kwa Ibn ‘Abbaas kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alimuona Allaah سبحانه وتعالى moja kwa moja. Ni kuwa alimuona kwa moyo si kwa macho, Kauli ya kwanza haipingani na ya pili.” Kisha akasema: “Ama kuhusu kauli yake Allaah سبحانه وتعالى katika Suratu An-Najm (53: 8).

“Kisha akakaribia (kwa Mtume) na akateremka.”

Huko siko kule kukaribia ambako kumetajwa katika kisa cha Al-Israa, Kwani kukaribia ambako kumo katika Suratu An-Najm, “Ni kukaribia kwa Jibriyl عليه السلام na kusogea zaidi kama alivyosema Mama wa Waumini ‘Aaishahرضي الله عنها na Ibn Mas’uud رضي الله عنه. Mtiririko wa maneno unafahamisha juu ya maana haya; “Amekukaribia na kusogea sana.” Katika Hadiyth ya Al-Israa, Kuna maana kuwa kukaribia huko ni kukaribia kwa Mola Mtukufu Aliyetukuka na kuwa karibu kwake zaidi. Hakuna kupingana katika Surat An-Najm. Lakini kutajwa huko ndani yake ni kuwa yeye alimuona mara nyingine mbele ya Sidratul-Muntahaa, Na huyo ni Jibriyl عليه السلام.



Mtume Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم alimuona Jibriyl عليه السلام katika sura yake halisi mara mbili; ya kwanza hapa duniani na mara nyingine katika Sidratul-Muntahaa na Allaah سبحانه وتعالى Ndiye Mjuzi zaidi.


Lilituka lile tukio la Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kupasuliwa tena kifua chake kwa mara ya pili. Kwa ujumla katika safari hii aliona mambo mengi; miongoni mwa hayo ni kule kuletewa maziwa na pombe na kuchagua maziwa badala ya pombe, Na pakasemwa, “Umeongozwa katika fitrah na umechagua na kupata fitrah, Ama kwa hakika laiti ungechukua pombe Ummah wako wote ungepotea, “Katika safari hiyo alionyeshwa mito minne huko peponi, Mito miwili iko nje na mito miwili iko ndani. Mito miwili iliyo nje ni mito ya Nail (Nile) na Furaat (Euphrates), Na maana ya mambo hayo ni kuwa ujumbe wake utafanya makazi yake katika majanga yenye rutuba katika Nail na Furaat na watu wake ndio watakaokuwa wasimamizi wa da’awah ya Kiislaam, Kizazi baada ya kizazi, na si kuwa maji ya mito miwili hiyo yanachimbuka kutoka peponi.


Alionyeshwa Malaika muangalizi wa moto wa Jahannam ambaye hacheki, mwenye uso usio na furaha wala bashasha. Alionyeshwa pepo na moto. Alionyeshwa walaji wa mali za yatima kwa dhulma, Waliokuwa na midomo kama ya ngamia, Wanatupiwa midomoni mwao vipande vya moto kama mawe na kisha kutolewa katika tupu zao za nyuma.


Alionyeshwa walaji wa ribaa waliokuwa na matumbo makubwa yaliyowafanya wasiweze hata kuondoka mahala walipokuwepo. Alipita na kuwaona watu wa Fir’awn wakionyeshwa moto na hali wakipita wakiukanyaga.

Alionyeshwa wazinifu, Mbele yao kulikuwa na nyama iliyonona vizuri na pembeni mwao kulikuwa na nyama duni iliyooza yenye uvundo. Wakawa wanakula ile nyama duni iliyooza yenye uvundo, na wanaiacha ile nzuri iliyonona. Alionyeshwa wanawake wanaonasibisha waume zao watoto ambao si wao (watoto wa zinaa) hawa walikuwa wametundikwa kwa matiti yao. Na aliona msafara wa kibiashara wa watu wa Makkah wakati wa kwenda na wakati wa kurudi kwake, Na aliwafahamisha watu hao juu ya ngamia aliyewatoroka na alikunywa maji yao yaliyokuwa yamefunikwa na hali ya kuwa wao wamelala na kisha akakiacha chombo kikiwa kimefunikwa na jambo hilo ndilo likaja kuwa dalili (hoja) ukweli wa madai yake asubuhi ya usiku wa Israa.


Ibnul Qayyim alisema. “Kulipopambazuka Mjumbe wa Allaah صلى الله عليه وآله وسلم akiwa kwa jamaa zake aliwaeleza yote Aliyoonyeshwa na Allaah Mtukufu Mwenye Kushinda, Miongoni mwa miujiza Yake mikubwa. Makuraishi walipinga na hawakutaka kabisa kuamini khabari hizo. Katika kutafuta ukweli wa maelezo yake walimtaka awaeleze ulivyo Msikiti wa Baytul Al-Muqaddas. Kwa uwezo wake Allaah سبحانه وتعالى Akamdhihirishia hiyo Baytul Al-Muqaddas machoni mwake, akawa anawaelezea alama zake moja baada ya nyingine na wakashindwa kukanusha kwa vile alikuwa akiwaambia ukweli. Mwisho akawaeleza kuhusu ule msafara wa wafanyabiashara aliokutana nao wakati wa kwenda na kurudi; akawaeleza ni lini msafara huo unategemea kufika; akawaeleza kuhusu ngamia aliyeuongoza msafara huo, Na mambo yakatokea kama alivyowaeleza. Hata baada ya kujulishwa yote hayo Ma-Quraysh walizidi kukanusha na kukufuru. Abu Bakr رضي الله عنه ameitwa “Swiddiyq” ‘Msadikishaji’ kwa sababu ya kulisadikisha tukio hili.


Yapo maelezo mafupi na marefu yaliyokuja katika kueleza sababu ya safari hii. Ipo pia kauli ya Allaah سبحانه وتعالى Mwenyewe inatosha kabisa kueleza sababu ya safari hii, Pale Aliposema:

“Ili Tumuonyeshe baadhi ya alama Zetu” (17:1).

Na huu ni utaratibu wa Allaah سبحانه وتعالى kwa Mitume, Pahala pengine ndani ya Qur-aan Anasema:
“Na namna hivi Tulimuonyesha Ibraahiym ufalme wa mbingu na ardhi (kuwa ni wa Mungu), Na ili awe miongoni mwa wenye yaqini.” [Al-An’aam: 75].


Na Alisema kumwambia Muusa عليه السلام:


“Tukuonyeshe miujiza (mingine) mikubwa mikubwa.” [Twaahaa: 23].

Na ameweka wazi makusudi ya huko kuonyeshwa, “Ili awe ni miongoni mwa wenye yaqini.” Kwa hivyo ni wazi basi kuwa elimu ya Mitume katika kumjua Mola wao inatokana na kuiona kwa macho miujiza Yake na kwa njia hiyo kuwa na yaqini na Allaah سبحانه وتعالى kwa kiasi kisichokuwa na mfano. Ni ukweli ulio wazi kuwa jambo la kujionea si sawa na la kusikia, Na hii ndio sababu Mitume عليهما السلام walivumilia mengi katika njia ya Allaah سبحانه وتعالى mambo ambayo si rahisi kuvumiliwa na watu wa kawaida. Nguvu zote za kidunia mbele ya Mitume ni kama ubawa wa mbu hawatishiki nazo hata chembe, Hata wanapofanyiwa vitimbi na wakati mwingine kuteswa.



Bila shaka msomaji ataona kuwa katika suratul Israa Allaah سبحانه وتعالى Amekitaja kisa cha Al-Israa katika Aayah moja tu, Kisha Akaingia katika kutaja fedheha za Mayahudi na maovu yao, Na kisha Akawazindua kwa kuwaeleza kuwa hii Qur-aan inaongoza kwenye mambo yanayohitaji misimamo madhubuti kabisa. Inawezekana msomaji akadhania hizi Aayah mbili hazina uhusiano wowote, Jambo hili si kweli, maana kwa maneno haya Allaah Mtukufu Anaashiria kuwa kwa hakika Israa ni tukio lilitokea Baytul Al-Maqdis na kuwa Mayahudi watanyang'anywa cheo cha kuwaongoza wanaadamu kutokana na matendo yao maovu ambayo wameyafanya. Matendo ambayo hayakubakisha nafasi ya wao kubakia katika cheo hicho na kuwa Allaah سبحانه وتعالى Atakihamisha cheo hicho kwa vitendo na kumkabidhi Mjumbe Wake Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم ambaye atamkusanyia vituo viwili vikuu vya Da’awah ya Ibrahiym عليه السلام. Wakati umefika wa kuhamishwa kwa uongozi wa kiroho kutoka Ummah ulioijaza historia yake kwa udanganyifu, Khiyana, Madhambi na uadui kwenda katika ummah mwingine utakaoaminika kwa wema na kheri. Mtume wa Ummah huo hakuacha kuwa anayesifika na wahyi wa Qur-aan inayoongoza kwenye msimamo ulio sahihi.

Kwa vipi utahama uongozi huu hali ya kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم anazunguka katika majabali ya Makkah hali ya kuwa ni mwenye kufukuzwana kupigwa na watu wa kabila lake? Suala hili linaibua ukweli mwingine ambao ni kuwa mzunguko wa kwanza katika Da’awah hii ya Kiislaam umekaribia kufika mwisho na kukamilika, Na baada ya hapo utaanza mzunguko wa kwanza katika mapito yake. Kwa sababu hiyo ndio maana tunaona kuwa baadhi Aayah zinakusanya mambo yanayohusu makhofisho ya wazi na makemeo ya kutisha dhidi ya Mushirikina.

“Na pindi tukitaka kuuteketeza mji huwaamrisha wale wenye starehe na taanusi, lakini wao huendelea kutenda maovu humo. Basi hapo kauli huthibiti juu ya mji huo, nasi tukauangamiza kwa maangamizo makubwa.


“Na kaumu ngapi tumeziangamiza baada ya Nuuhu! Na Mola wako Mlezi anatosha kabisa kuwa ni Mwenye kuzijua na kuziona dhambi za waja Wake.” [Al-Israa: 16-17].

Pamoja na Aayah hizi zipo nyingine zilizowaweka wazi Waislaam na zinazoendelea kuwawekea misingi ya maendeleo na kanuni zake na vyanzo vyake ambavyo hujenga jamii ya Kiislaam. Kama vile tayari wamekwishafika kwenye ardhi iliyo tayari, waliyapanga vizuri mambo yao kwa pande zote na wakaunda umoja wenye mshikamano madhubuti.


Katika jamii yao, hali kadhalika kulikuwepo na Ishara ya kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم atapata makimbilio na mahali pa amani ambako yatatulizana mambo yake na makimbilio hayo ndiyo yangekuwa kituo cha wito wake katika pande zote za dunia. Hii ni moja ya siri miongoni mwa siri za safari hii yenye kubarikiwa.

Tukio hili, ambalo kwa Muislam mwenye Iymaan barabara, hata kama lisingelikuwepo, Iymaan yake bado ingekuwa imara vilevile, ni tukio la kihistoria lenye kuzidisha kuujua uwezo wa Allaah سبحانه وتعالى na Utukufu Wake mkubwa usio na mithali. Ni tukio lenye mafunzo mengi ya kiimani na kiitikadi; ndani yake tumeona kumepatikana faradhi ya Swalaah, kumejulikana adhabu mbalimbali za matendo maovu ya hapa ulimwenguni, na hilo litaweza kutusaidia sana sisi kujiepusha na maovu hayo ili tusiishie kutumbukia ndani ya adhabu hizo kali. Tumeona utukufu na uzito wa Maswahaba kama Abu Bakr رضي الله عنه, na imetuzidishia heshima kubwa juu ya watukufu hao na kujua nafasi yao kubwa katika moyo wa mbora wa viumbe, kipenzi wa macho yetu, Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم. Tuchukue mazingatio yanayopatikana humo na kuyafanyia kazi katika maisha yetu na si tukio hili liwe la kuhadithiwa tu na watu kukusanyana kukisherehekea inapofika mwezi wa Rajab ambao kama tulivyoona mwanzoni kuna utata wa tukio hilo kuwa katika mwezi huo.


Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.