بسم الله الرحمن الرحيم

kutafuta elimu ni faradhi kwa kila muislamu
الحمد لله الذي نستعينه ونستغفره ونعوذ بالله من شرور أنفسنا ومن سيئات أعمالنا من يهد الله فلا مضل له ومن يضلل فلا هادي له .



ونشهد أن لا إله إلا الله وحده لا شريك له ونشهد أن محمدا عبده ورسوله أرسله بالهدى ودين الحق ليظهره على الدين كله وكفى بالله شهيدا




Sunday, July 4, 2010

FUNZO KWA VIJANA

Allaah Atakuajiri…Tawakkal Kwake!
Kijana mmoja alimaliza kusoma katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Madiynatul-Munawwarah na alikuwa mfano wa pekee kwa uhodari wake na mwenye akili nyingi alimaliza na kutunukiwa Shahada yake nzuri na akiwa na vyeti vinginevyo vya mapendekezo.
Lakini akazunguka kutafuta kazi katika kila shirika, na idara za serikali bila ya kufanikiwa kupata kazi popote.
Na kwa vile alitamani na kuazimia kuwa hatotoka katika uzuri wa vizuri. Nao ni mji huu mtukufu wa Madinatul-Munawwarah, kwani je, nani anayeonja maisha mazuri kabisa katika uzuri na mazuri ya mji huu wa mpenzi (wetu Mtume صلى الله عليه وسلم ) kisha akataka kuyawacha? Naye anaona makumbusho ya Mpenzi Mustafa صلى الله عليه وسلم na Maswahaba zake رضي الله عنهم katika kila shibiri ya mji huu? Kwani alitamani kuishi Madina akitumaini na kutegemea kupata fadhila za hadithi ya Mtume صلى الله عليه وسلم aliyosema :
((Atakayeweza kufia Madinah afanye hivyo kwani mimi nitamuombea shufaa atakayefia hapo))
Akaenda kwa mmoja wa walezi wema na miongoni mwa masheikh wema ambaye anayemuona humkumbusha Allaah سبحانه وتعالى, na anayemsikia sauti yake utajua kwamba ana khofu ya Allaah سبحانه وتعالى wala haifai kumtukuza mtu isipokuwa Allaah سبحانه وتعالى .
Kasema: "Nilikwenda kwake nikamwambia "Ewe Sheikh je, humjui mtu wa kuniajiri kazi? Kwani milango imefungika mbele yangu, wala haujabakia mlango nisiougonga na yote haikufaa kitu. Wala sitaki kutoka katika mji huu wa Madiynah". Sheikh akasema kwa lafudhi yenye kujiamini “Mwenye kuwa na yakini na ahadi ya Allaah, naam Wallaahi namjua nani wa kukuajiri".
Kwa haraka kabisa nikasema (huku furaha yangu ikidhihirika). Nani huyo ewe Sheikh? Mwenyeezi Mungu Akuzidishie mema. Nani huyo? Akasema Sheikh: "Huyo ni Allaah "عز وجل
Nikapigwa na bumbuwazi!
Akanitizama Sheikh akasema : "Ajabu! Ningelikwambia kuwa ni Waziri fulani na mhusika fulani ungelifurahikiwa na kuona ni kheri. Lakini nilipokutajia Yule Ambaye Anamiliki funguo za kila kitu na Yeye ndiye Muweza wa kila kitu, Ambaye Anamiliki vyote vya mbingu na Ardhi na khazina za mbingu na ardhi, naona uso wako umebadilika kama vile kwamba una shaka na ahadi ya Allaah سبحانه وتعالى Ambaye amesema"
((وَفِي السَّمَاء رِزْقُكُمْ وَمَا تُوعَدُونَ))
{{Na katika mbingu ziko riziki zenu na mliyo ahidiwa}}
Adh-Dhariyaat 22
"Nenda ewe mwanangu kwenye msikiti wa Mtume صلى الله عليه وسلم kabla ya Alfajiri kwa saa moja umkaribie Allaah تعالى katika thuluthi ya mwisho ya usiku (katika masaa ya kabla ya Alfajiri) na mimi nina hakika na kutumainika kwamba Allaah Atakutimizia amri (haja ) yako.
Akasema (kijana): “Nilitahayari na kuona haya kabisa, tahayuri ambayo sijawahi kuihisi kabla. Nikamuaga Sheikh kisha nikaondoka"
Nikaegesha kengele ya saa yangu kuniamsha saa tisa baada ya nusu ya usiku wa manane nikamka nikatawadha, kisha nikaenda Masjidi-An-Nabawi mtukufu huku nimejaa joto la imani ambalo siwezi kulielezea.
Nilipoingia, nikaswali ilivyopasa nikataka kunyanyua mikono yangu mbinguni niombe, lakini sikuweza kwa kuzidiwa na kilio ambacho kilinizidi nguvu hata nikadhania kuwa roho yangu itatoka na huku nikiwaudhi walio karibu yangu. Nikamuomba Allaah سبحانه وتعالى maneno machache na Allaah سبحانه وتعالى ndiye Ajuaye yaliyomo vifuani.
Nikaswali Swalah ya jamaa ya Alfajiri kisha nikahudhuria darasa la mmoja wa wanachuoni wetu wenye kuheshimika kisha nikaelekea nyumbani kwangu. Nikawa nimesahau kila kitu isipokuwa Allaah سبحانه وتعالى wala sikujiandaa kufikiri au kupanga chochote katika mambo ya dunia siku hiyo
Wakati niko njiani nikahisi kama mtu akiniambia elekea njia hiyo nyingine. Nikaelekea huko, mara nikakuta ofisi ya Idara ya serikali ambayo sijawahi kabla kuipitia. Nikasema rohoni 'kwa nini nisiende nikawaulize kama wanayo kazi waniajiri?"
Nikaingia, kisha nikamkabili bwana mmoja aliyetabasamu usoni kwangu aliponiona naye wala hanijui.
Nikamuuliza: "Ewe ndugu yangu mimi simjui mtu hapa, lakini ukipenda kupata thawabu, hivi hapa vyeti vyangu na shahada zangu, hakika mimi siku nyingi natafuta kazi sijafanikiwa. Alipotazama shahada zangu akaegemea pembeni mwa maktaba yake kwa mikono yake, akainuka na kunitizama akasema: "Subhana Allaah! muda mrefu sisi tunatafuta watu wanaomiliki elimu kama hii uliyonayo, ulikuwa wapi? umekuja kutoka wapi? Sasa hivi utapata kazi Insha Allaah!"
Akasema (Kijana): 'Nikainuka kitini nikamsujudia Allaah سبحانه وتعالى sajda ya kumshukuru hapo hapo ofisini kwake huku machozi yakinilenga machoni mwangu na huku nikimkumbuka yule Sheikh mwema na yakijirudia maneno yake, “Huyo ni Allaah عز وجل , Huyo ni Allaah عز وجل"
Kisa hiki ni cha kweli. Na ingawa ni kifupi, lakini utaona kwamba kina mafundisho mengi yenye manufaa kwetu:

1. Kuwa na Tawakkul na Yakini Na Allaah سبحانه وتعالى
2. Sio hoja kusoma na kupata Shahada bali Allaah سبحانه وتعالى Ndiye Mwenye Kumruzuku mtu.
3. Kuupenda mji wa Madinatul-Munawwarah na kupata fadhila zake.
4. Ni vizuri sana kutafuta Nasiha/ushauri kutoka kwa watu wema.
5. Moja ya nyakati nzuri za Du’aa ni katika nyakati za kabla ya Alfajiri (Swalatu-Tahajjud)
6. Swalah ya Jamaa msikitini haswa alfajiri ni muhimu.
7. Kulia kwa sababu ya Allaah سبحانه وتعالى humkurubisha mtu zaidi kwa Allaah na humuongezea imani na mapenzi ya Allaah سبحانه وتعالى
8. Kusujudu sajdah ya kumshukuru Allaah سبحانه وتعالى kila unapopata au unaposikia jambo jema.
9. Kuweka Nia ya jambo jema Allaah سبحانه وتعالى Atakuonyesha njia.

Zifuatazo ni aya zenye kutufundisha faida ya Kutawakkal kwa Allaah, na kuwa Wacha Mungu.
(( وَمَن يَتَّقِ اللَّهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا))
{{Na anaye mcha Mwenyezi Mungu humtengezea njia ya kutokea}}
At-Twalaaq: 2
(( وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لاَ يَحْتَسِبُ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّهِ فَهُوَ حَسْبُهُ إِنَّ اللَّهَ بَالِغُ أَمْرِهِ قَدْ جَعَلَ اللَّهُ
لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا))
{{Na humruzuku kwa njia asiyotazamia. Na anayemtegemea Mwenyezi Mungu Yeye humtosha. Hakika Mwenyezi Mungu anatimiza amri yake. Mwenyezi Mungu kajaalia kila kitu na kipimo chake}} At-Talaaq: 3
(( وَمَن يَتَّقِ اللَّهَ يَجْعَل لَّهُ مِنْ أَمْرِهِ يُسْرًا ))
{{Na anaye mcha Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu humfanyia mambo yake kuwa mepesi}} At-Talaaq : 4
Allaahumma tujaalie tuwe wacha Mungu, wenye kutawakkal Kwako daima, Utusahilishie mambo yetu, na Uturuzuku kheri nyingi. Aamiin.

VIDOKEZO MUHIMU KWETU

Vidokezo Muhimu Kwa Wazazi Wenye Wasichana Na Wavulana


((Tumejitahidi kurekebisha baadhi ya majina na usemi ili makala ifahamike vizuri na Jamii yetu))

NINI WAZAZI WAFANYE ILI VIJANA WAO WAWE NI WAISLAMU WENYE KUTEKELEZA UISLAMU KWA VITENDO?


1. Yatilie Bidii Malezi Kuliko Hata Kazi Yako Ya Kutwa Nzima
Hii ina maana kwamba wazazi wote wawili ni lazima waelewe kuwa watoto wao ni wa kweli kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), na baba atakuja kuulizwa vipi kawalea watoto wake. Ikiwa watoto wao hawatokulia katika kuutekeleza Uislamu kwa sababu ya mapuuza ya wazazi wao, halitokuwa ni jambo la kukubalika kwa maisha ya hapa duniani na hata ya baadae.


2. Punguza Au Badilisha Masaa Ya Kazi Kwa Ajili Ya Kupata Muda Wa Kuwa Pamoja Na Familia Yako
Ni bora kuwa na kazi moja yenye muda wa kudumu, anasa chache katika nyumba (yaani sio magari mengi, nguo za gharama nyingi, nyumba kubwa ya fakhari, televisheni kila pahali), na muda zaidi wa kuwa pamoja na familia, kuliko kuwa na mambo mengi ya anasa na kukakosekana malezi. Haya yote yanawahusu mababa na mamama. Wazazi hawawezi kuwafunza watoto wao bila ya wao kuwepo nao kikawaida. Acha kazi za ziada kwenye siku za mwisho wa wiki au kazi za jioni na badala yake nenda na watoto msikitini kwa ajili ya Halaqah (darsa za dini) na shughuli nyenginezo. Au tilia maanani kugeuza nyakati za kazi ili uwe nyumbani wakati ambao watoto wapo.


3. Soma Qur-aan, Ifahamu Maana Yake, Angalau Kwa Dakika Tano Kila Siku
Angalau dakika tano. Inawezekana ikawa kwenye gari wakati (umesimama kwa ajili) ya msongamano wa magari, mapema baada ya Swalah ya alfajiri, au mara tu kabla ya kulala, soma Qur-aan pamoja na maana au tafsiri. Baadae angalia umuhimu wa taathira yake. Insha Allaah utajikurubisha kwa Allaah, na baada ya muda mrefu, utakuwa mfano bora wa kuigwa na kuisaidia familia nzima kujikurubisha kwa Allaah vile vile.


4. Hudhuria Halaqah Kila Wiki
Fanya biashara ya kubadishana mchezo wa karata, au kuangalia televisheni siku za jumapili kwa kuhudhuria Halaqah (darsa duara za dini; ima misikitini au majumbani au kwenye kumbi za kukodishwa). Ikiwa (katika Msikiti) hakuna utaratibu uliowekwa tayari kwa wakati huo, basi msaidie Imamu ili auweke. Hudhuria kwa uangalifu Natija ya kufanya haya ni kule watoto kuwaona wazazi wao wanafanya bidii ya kuusoma Uislamu, na wao kwa namna yoyote ile watapata hamu ya kufanya vile vile (wafanyavyo wazazi wao).


5. Waheshimu Watoto Wako
Kuwaheshimu watoto wako ina maana usiwafanye kama wapumbavu, bali ni kuwachukulia kama wao ni watu wazima, usiseme nao kitoto au kuwafedhehesha na kuwatukana. Wajumuishe kwenye shughuli za nyumbani zenye manufaa na waombe ushauri kwenye maamuzi ya mambo muhimu.


6. Kuwa Na Hamu Ya Kushiriki Katika Mambo Wanayoyafanya
Je, Faatwimah anacheza hockey ya wasichana watupu kwenye mashindano? Hudhuria michezo yake kikawaida pindi ikiwezekana. Je, 'Aliy anakusanya stampu? Tafuta ikiwa unaweza kupata stampu za barua za zamani za wazazi wako kutoka Tanzania au Kenya na umpatie. Je, 'Umar anapenda kutengeneza tovuti (websites)? Tembelea tovuti yake, mtumie barua pepe (e-mail) ya kumpongeza kupitia sehemu ya ujumbe na mpe baadhi ya rai katika sehemu za tovuti yake. Mpe kitabu cha maarifa ya juu ya kusanifu tovuti kama ni zawadi ya 'Iyd.


7. Yatambue Matatizo Yaliyopo Na Wajulishe Wazi Wazi
Kwa kadiri unavyotumia wakati wako kuwa pamoja na vijana wako, utakuwa na uwezo zaidi wa hisia ya kugundua kitu gani kinawakera Usifagilie hisia hii chini ya zulia (usiufiche ukweli). Ujulishe kwa uwazi. Lakini usifanya kwenye mkutano wa familia au mbele ya wengine. Fanya hivyo wakati wa fikra inayofuata.


8. Weka Miadi Ya Kuonana Na Kijana Wako
Kwa vile mara nyingi uwekaji wa miadi ya kuonana inahusishwa na kukutana kwa msichana na mvulana, wazo hili linaweza kutumiwa kwa aina yoyote ya mkutano baina ya watu wawili wanaotaka kutambuana vyema.
Ni muhimu sana kuweka miadi ya kuonana na vijana wako katika kiwango tofauti mara wanapoingia kwenye umri wa usichana/uvulana kwa sababu wao si watoto wadogo tena. Unaweza kuweka miadi na Sumayyah wakati anapomaliza masomo yake ya sekondari (badala ya kwenda kwenye sherehe za ngoma), Yaasir naye wakati anapopata leseni yake ya kuendesha gari au ikiwa unahisi kuna kitu kinawakera na unataka kuwajulisha peke yao ili kuwasaidia kutatua mashaakil yao.


9. Usiwe Tu Ni Mzazi Kwa Mtoto Bali Uwe Pia Ni Rafiki Kwake
Kujenga urafiki nae ina maana ya kuwapa majukumu katika familia. Mpe mvulana wako wa miaka 16, 'Uthmaan, ambaye ana leseni ya gari, majukumu ya kumsaidia mama yake siku za jumamosi anapokwenda madukani kununua vyakula. Mpe msichana wako wa miaka 15, Khadijah, ambaye anapenda maua, kuwa ni mwangalizi wa bustani pamoja na kukatakata majani. Kwa njia hii vijana watajihisi kuwa na wao ni sehemu ya familia, wanajumuishwa na wanahitajiwa.


10. Jenga Msikiti Katika Nyumba Yako (Tenga Sehemu Maalum Ya Kuswalia Ikiwezekana)
Chagua sehemu ya chini ya nyumba yako au katika ukumbi wako uwe ni msikiti wa nyumbani. Itayarishe hiyo sehemu kwa kuweka miswala, misahafu na iwe sehemu khaswa ya kuswaliwa.
Fanya msikiti huu kuwa waangalizi wake ni watoto tu peke yao. Muweke mkubwa wao kuwa ni msimamizi na mpangaji wa majukumu kwa wadogo zake. Majukumu hayo yawe ni pamoja na kuuweka msikiti uwe safi, kuwaamsha watu alfajiri, kuadhini, na kadhalika.


11. Usijenge (Fikra Kuwa) “Uislamu Ni Kwa Wanaume Tu”
Hii ina maana usibague wake zako na wasichana kwenye Swalah. Wakati wanaume wanaposwali Swalah ya jama'ah, hakikisha wanawake wapo nyuma yao au wanaswali Swalah ya jama'ah (sehemu nyengine) na wao. Vile vile hakikisha Imamu anasoma kwa sauti kiasi ya kusikika na wanawake ikiwa wapo sehemu nyengine ya nyumba. Vile vile wahimize wanawake waswali Swalah ya jama'ah pindi ikiwa wanaume hawapo nyumbani.


12. Anzisha Maktaba Ya Kiislamu Na Chagua Muangalizi Wake
Iandae nyumba yako yenye maktaba ya Kiislamu kwa vitabu, video na kanda za kusikiliza zenye maadili ya Kiislamu, mpatie kila mmoja kwa mujibu wa umri na hamu yake. Ikiwa 'Abdallah mwenye umri wa miaka 13 anapenda vitabu vya hadithi za hatari, kwa mfano, hakikisha unavyo vitabu vya Kiislamu vya kila aina vyenye hadithi za aina hiyo.
Mfanye mmoja katika vijana wako kuwa ni mwangalizi wa maktaba. Aipangilie na kuiweka katika hali nzuri. Kitu chochote kinachotakiwa kuingizwa kwenye maktaba ni lazima kipitishwe kwake. Mpe msimamizi wa maktaba bajeti ya kila mwezi ya kununulia vitabu, kanda za kusikiliza na kadhalika.


13. Wachukue kwenye shughuli za Kiislamu
Badala ya kwenda kwenye mgahawa (restaurant) kwa ajili ya vyakula vya kila aina, hifadhi pesa zako kwa ajili ya kumchukua kila mmoja katika chakula au shughuli za jamii ya Kiislamu. Fanya bidii kwenda kwenye matukio ambayo vijana wengine wa Kiislamu watahudhuria na kutakuwa na msemaji atakayetoa ujumbe kwenye mkusanyiko (huo).
Ni muhimu vile vile kufanya mazoea ya kumchukua 'Abdur-Rahmaan na 'Aishah kwenye kambi za Kiislamu na mikutano ambayo watakutana na watoto wenzao wa Kiislamu kwa wingi na wenye umri unaolingana na wao.


14. Hamia Kwenye Maeneo Yenye Waislamu Wengi
Wazo hili limekusudiwa haswa kwenye eneo lilo karibu na msikiti. Hatua hii ni muhimu kwa kuwa watoto wako ili wawe wanaambatana na watoto wengine wa Kiislamu wenye umri ulio chini, sawa au zaidi na wao, katika mambo yao ya kimsingi ya kila siku.


15. Wasaidie Vijana Wako Ili Waanzishe Wao Wenyewe Kikundi Cha Vijana
Baada ya kuwa unaishi kwenye eneo la Waislamu na unahudhuria shughuli za Kiislamu kikawaida, vijana wako katika mambo mengi wataukuza urafiki na Waislamu wengine wenye umri unaolingana na wao. Usiyaachie haya yakaishia hapo.
Wasaidie kuanzisha kikundi cha vijana, sio tu kwa ajili ya kusoma Uislamu bali pia kutembea pamoja kwenye viwanja vya kupendeza, kuogelea, na kadhalika. Kuwepo na mikutano kwenye nyumba za wanachama (vilabu vya Kiislam) kila wiki au mara mbili kwa mwezi. Kihusishe kikundi hichi kwenye kazi muhimu kama za kusafisha takataka msikitini au kuhudhuria nyumba zinazolelewa wazee. Kikundi hiki ni lazima kiwe na uangalizi wa wazazi, ijapokuwa maamuzi ya vijana yasiingiliwe mpaka ionekane kikweli kweli upo umuhimu/haja ya kufanya hivyo.

16. Anzisha Utaratibu Wa Televisheni Huru Kwa Wakati Wa Jioni Na Kuwepo Msimamizi Wakati Wote Wa Kuangalia Televisheni
Mshindani mkubwa wa wazazi juu ya umakini kwa watoto wao ni uangaliaji wa televisheni. Uangalizi madhubuti uwepo juu ya maelekezo ya televisheni. Kuwa makini na kila kinachoangaliwa na kila mmoja wao, ina maana ya kuchukua tahadhari ya kuwakumbusha na kuwasaidia ili kila mmoja ajiepushe na kuangalia filamu za ngono, misalsal (filamu za kuendelea), na filamu zisizotilia hima shughuli za Kiislamu. Weka orodha kwenye ukuta pembezoni mwa televisheni ya vipindi vinavyokubaliwa na visivyokubaliwa.
Kuanzisha televisheni huru wakati wa jioni ina maana ya kuwa, kuwepo jioni moja kwenye wiki ambapo kutakuwa hakuna yeyote kati ya watu wazima, vijana au watoto atakayeruhusiwa kuangalia televisheni. Hii ni kwa kutarajia kwamba itakuwa ni hatua ya mwanzo ya kupunguza televisheni kwenye nyumba. Huu ni wakati muwafaka wa kuutumia kwa kidokezo kifuatacho.


17. Kuwepo Mikutano Ya Familia Kwa Kila Wiki
Madhumuni ni kutafuta kinachoendelea katika maisha ya kila mmoja wao na kutoa ushauri wa mambo muhimu katika familia. Hafswah ameanza kuhudhuria Halaqah, Hasan naye amerejea kutoka kwenye kambi ya Kiislamu, na Husayn amekaribia jaribio lake la mwisho katika hesabu za algebra. Sio tu kutoa taarifa kwa mfumo wa muhtasar, bali ni kujadiliana na kuwasiliana baina ya kila mmoja, na kuweka taarifa mpya kabisa kwa kila kinachoendelea katika maisha ya kila mmoja wao, ambapo inakuwa ni vigumu (kuyafanya haya) pale watoto wanapokuwa wanakaribia kuingia kwenye umri wa ujana.
Huu vile vile ni wakati wa kuishauri familia na kuamua juu ya mambo makubwa yanayomuathiri kila mmoja kati yao kama kuhamia mji mwengine, harusi ya mmoja kati yao, iwapo yupo mwenye wakati mgumu skuli kwa sababu ya wanao mbughudhi, na kadhalika.
Tafadhali kumbuka: Mashauriano katika familia haimaanishi kwamba maamuzi ya walio wengi ndio yafuatwe kuhusu hali inayojadiliwa. Bali wazazi watabaki kuwa ndio wenye dhamana, fikra na rai za vijana na watoto wadogo, wazazi watayazingatia kwenye kufanya maamuzi yao ya mwisho.


18. Weka Kigezo Cha Majukumu - Nini Abu Bakr Kafanya?
Mbali ya kuwa wewe mwenyewe ni kigezo juu ya kuutekeleza Uislamu kwa vitendo, hakikisha unawawekea vijana wako vifaa vya kusoma kuhusu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) na Maswahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum), wote wanawake na wanaume, la sivyo, huenda watoto wako wakaiga wahusika wa vipindi vya televisheni ambavyo watoto wako wanaangalia na wakawa ndio Maswahaba wao.
Jadiliana nao nini Maswahaba walikuwa wakifanya katika kukabiliana na maisha ya vijana. Swahaba Abu Bakr asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu) angelifanya nini pindi angelimuona mtu anauza majawabu ya mtihani wa mwisho ya hesabu za darasa la saba au darasa la kumi na mbili (form IV)? Na 'Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) angelifanya nini pindi angelikabiliana na mtu mwenye kudanganya wazazi wake?


19. Soma Vitabu Kwa Ajili Ya Malezi Ya Uhakika
Hivi vinaweza kuwa ni vitabu vilivyoandikwa na Waislamu, lakini vitabu vilivyoandikwa na wasiokuwa Waislamu pia vinaweza kusaidia. Hata hivyo, jitayarishe na pia hakikisha kuwa unao uwezo wa kugundua ni vitabu vipi vinakubalika Kiislamu dhidi ya visivyokubalika.


20. Waache Waoe/Waolewe Mapema
Fitna kutoka nchi za Magharibi zimeeneza picha za ngono kwenye televisheni, mabango ya matangazo, mitaani, kwenye mabasi, katika filamu za maigizo, na kadhalika, nazo zinapatikana wazi katika baadhi ya nchi zetu. Inakuwa ni ngumu kwa kijana wa Kiislamu kuyakabili haya bila ya kuwa na matamanio na kushindwa kujizuia na maovu hayo. Ni jambo la maana kuwaacha waoe/waolewe mapema (Soma baadhi ya vidokezo vinavyowahusu wazazi juu). Hii itarahisisha shinikizo, na hapana haja ya kukatisha masomo yao kwenye suala hili.
Kumbuka, kama ni mzazi utabeba jukumu ikiwa mvulana au msichana wako atataka kuoa au kuolewa na wewe ukamkataza na akaishia kwenye kufanya uzinifu. Vile vile ni lazima ukumbuke kuwa unapotekeleza hatua hii usimlazimishe mvulana au msichana wako kuoa au kuolewa na mtu asiyempenda.


21. Mwisho Lakini Pia Muhimu - Omba Dua
Omba Dua. Ni yeye Allaah Pekee Anayeongoa au Kutoongoa, lakini ikiwa umetekeleza wajibu wako kama ni mzazi kuwafanya watoto kuwa ni wenye kuutekeleza Uislamu kwa vitendo, InshaAllaah, ni rahisi kuwalea kuliko kulipuuza jukumu hili. Pia waombee Dua vijana wako mbele yao. Kufanya hivyo kutawakumbusha wao jinsi gani unavyowapenda na kujihusisha nao.


Du'aa Mojawapo Katika Qur-aan
رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا
Rabbanaa Hab-Lanaa Min Azwaajinaa Wa-Dhurriyaatinaa Qurrata A'yuniw-Waj'alnaa Lil-Muttaqiyna Imaama.
((Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na Utujaalie tuwe waongozi kwa wacha Mungu)) [Al-Furqaan: 74]