NA KHALID BILAL
Assalaam alykum,
Hivi karibuni kumezuka tiba ya ajabu ambayo imewashangaza wengi kitaifa na hata kimataifa, tiba hiyo ambayo ipo kiimani zaidi kutokana na madai ya hao wanaotoa tiba hiyo kudai kuwa wameoteshwa na Mungu/bikira maria/krsito/mizimu pia kufanikiwa kwa tiba hiyo kunategemea na imani ya mtu juu ya tiba hiyo kuwa inaponya, pia wanadai kuwa tiba hii inatibu magonjwa sugu ya aina yoyote kama vile kansa, presha, kisukari, ukimwi na mengineyo.
Cha kushangaza zaidi juu ya tiba hii ni juu ya asili ya tiba hiyo na kwamba tiba hii haina dozi, ni kikombe kimoja mpaka viwili na ugonjwa wako huondoka lakini pia tiba hii hupatikana kwa kuchemshwa mmea ambao kwa baadhi ya jamii mmea huo hujulikana kama ni sumu.
Nao watanzania wajikuta wanaipokea tiba hii moja kwa moja bila kujiuliza na kufikiria kwa umakini ukweli na undani wa tiba hii, kuna baadhi ya waliopata tiba hiyo wanadai wamepona na wengine wanadai bado hawajapona. Nayo serikali ya Tanzania yaingilia mambo ya kiimani na baadhi yao kupelekea kuingiliana katika majukumu ya uongozi pia viongozi wa dini nao hawakuwa nyuma katika hili. Haya yote si kwamba nimeyatoa kichwani bali ni kupitia ushahidi wa magazeti mbalimbali na usikilizaji wa redio. Ngoja tuanze kujua undani wa:
TIBA YA BABU LOLIONDO
Mchungaji Mstaafu wa KKKT (Babu), Ambilikile Mwasapile, umri (78) aishie kijiji cha Samunge, Loliondo, wilaya ya Ngorongoro, mkoa wa Arusha. Ni mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini na Kati, ambapo alitumikia utumishi huo kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20, alifanya kazi hiyo kwa uadilifu uliotukuka na kazi yake imekuwa mfano wa kuigwa na wengine mpaka leo. Mchungaji huyu mstaafu alianza kutoa tiba ya kikombe Agosti 2010 huku akisema hadharani wala hakusema kwa siri kuwa dawa yake imepata uponyaji wa kimungu, kwa maana kuwa kinachoponya sio ile dawa bali ni neno la Mungu kwenye ile dawa. (Gazeti la Tanzania daima 30-03-2011)
Mchungaji huyo alisema “Nimefanya kazi za uchungaji tangu mwaka 1967 katika sehemu kadhaa nchini hadi mwaka 1989 nilipohamishiwa katika eneo hilo. Na nimefanya kazi za uchungaji hapa hadi nilipostaafu mwaka 2002”. (Gazeti la Raia mwema 16-03-11)
Pia alisema “Nilianza kuota maono na kusikia sauti ya Mungu tangu mwaka 1991 ikinieleza kuwa nibaki kuishi eneo hili; kwani Mungu alikuwa anataka kunipa kazi maalumu ambayo kwa wakati huo sikuifahamu” (Gazeti la Raia Mwema toleo 176)
Mchungaji Mwasapile amewaambia waandishi kwamba dawa hiyo alionyeshwa na Mungu, na kwamba yeye anakawaida ya kuzungumza na Mungu mara kwa mara. Anadai pia kwamba Mungu ndiye aliyemwambia kwamba aitoze TSh.500/= kwa kila mgonjwa anatakayempa kikombe cha dawa hiyo ambayo ni ya kikombe kimoja cha maji yaliyochemshwa ya mizizi ya mti unaoitwa mugariga au muugamuryaga (kwa lugha ya Kisonjo). Na magonjwa anayotibu ukimwi, kisukari, saratani, kansa, , shinikizo la damu (presha), kifafa na magonjwa mengine sugu ambayo yamekuwa yakitishia uhai wa maisha ya Watanzania wengi.(Gazeti la Raia Mwema 22-03-11)
KHALID: Hapa ni wazi kuwa tunataka tubadilishwe imani zetu bila ya wenyewe kujua, hakuna mwenye uwezo wa kuzungumza na Mungu isipokuwa Mitume na Manabii nao wameshaisha/wameshafariki, Je huyu ni Mtume/Nabii au TAPELI? Huu ni mpango wa kanisa katika kutufanya tumshirikishe Mungu, yani tuwe WASHIRIKINA.
Inaendelea, Gharama ya tiba hiyo ni Tsh 500/= ambapo Tsh 200/= ni kwa ajili ya kanisa, Tsh 200/= kwa ajili ya kuwalipa wafanyakazi wake na 100/= ndo yake binafsi, Lakini hata hiyo, Sh 100 ambayo inakwenda kwake haitumii, kwa sababu anasema kila kitu kuhusiana na dawa hiyo ni kwa mujibu wa maono aliyopewa na Mungu, hivyo hata hizo Tsh100/= hatazitumia hadi pale Mungu atakapompa maelekezo. Ni mti huo huo unaotumiwa na Babu wa Loliondo kuponya ambao Wagogo wao huutumia kama sumu kwenye mishale yao; wenyewe wanauita “usungu”! (Gazeti la Raia Mwema 30-03-2011)
Baadhi ya majina ya mmea wa babu ni pamoja na angelica archangelica, na jina jingine linalorushwa ni mmea wa Carissa edulis na jina ambalo limetushtua wengine ni lile la mmea wa antiaris toxicana. Mimea yote hiyo mitatu ina sifa za madawa.
Mmea wa Carisa edulis - nao una sifa kadha wa kadha za kimadawa Kuanzia mzizi, magamba na majani yake yote yana sifa ya kutumika kimadawa. Na umetumika sehemu nyingi duniani kama tiba vile vile, Baadhi ya sifa zake nayo ni kutumika kupunguza maumivu. Unaweza pia kusaidia kutibu saratani na magonjwa mengine.
Mmea wa angelica archangelica - unajulikana sehemu mbalimbali duniani kutumika katika tiba za mitishamba, na watu kadhaa katika historia wamewahi kudai kuoteshwa ndoto juu yake ili wautumie kwa ajili ya uponyaji tangu karne ya 12, Baadhi ya sifa zake za kitabibu ni pamoja na kupunguza maumivu, na kusisimua mfumo wa kinga za mwili na hata kushambulia maambukizi ya bakteria na virusi.
Mmea wa antiaris toxicana - huu hujulikana kama mkuki wa sumu. Unajulikana hivyo kwa sababu tangu kale sumu yake imekuwa ikitumiwa kuweka kwenye mikuki na mishale kwa ajili ya mapigano na inadaiwa ni sumu kali sana. (Gazeti la New Habari 21-03-11)
Babu amesikika akisema yafuatayo, kuna watu ambao wameanza kuwaambia vijana wa huku kwetu ambao wanajua miti hiyo tunayoitumia kwamba wawachimbie, na wapo ambao wameshachimbiwa tayari kwa lengo la kwenda kutengeneza dawa. Akaendelea kusema:
“Sasa nawambia ya kwamba si kweli, huo ni wizi sikubali mtu yoyote mahali popote kupewa dawa na mtu kwamba mimi nimeitambua dawa hiyo, Mungu hakuagiza hivyo, naomba taifa letu lijaribu kuwatangazia mataifa mengine kuwa dawa ya aina hiyo haitakuwa dawa, hadi pale Mungu atakapoagiza vinginevyo.
“Kwa wakati huu amemruhusu mtu mmoja tu ambaye ni mimi kutoa dawa hii, nitakapochimba dawa hiyo na mwingine akachimba, Mungu ameniambia kuwa ya huyo mtu si dawa, kwa hiyo watu wasidanganywe na matapeli”
“Kuhusu masharti ya dawa hakuna, ila mimi nimeweka sharti moja, si Mungu, nawaambia watu kwamba ukitumia dawa hii basi kama wewe ni mtumiaji wa pombe usinywe siku uliyokunywa dawa na kama sharti hili lisingekuwa sawa, basi Mungu angeniambia.”
“Nimesema hivi dawa nnayotoa ina nguvu za Mungu, kwa hiyo inashika pahala pa dawa alizokuwa akitumia mgonjwa, sasa ni hiari ya mtu kuendelea kuzitumia au kuziacha. Pia dawa hii inatibu kila ugonjwa maana watu wameniletea taarifa walipopona ugonjwa fulani,wamesema hata magonjwa mengine waliyokuwa nayo yamepona, lakini pamoja na hayo sio kinga, ni ya kutibu aje mtu ambaye ni mgonjwa anaumwa”. (Gazeti la New Habari 21-03-2011)
KHALID: Mbona mambo mengine anajiamulia yeye mwenyewe bila ya kuambiwa na Mungu? Kama tiba ni mti na si imani mbona anawazuia watu wasiutumie? Hapa ASITUDANGANYE, tiba hii ni ya imani ya kikristo na si mti, hivyo tukimfuata tutakuwa tumefanya shirki tena shirki kubwa.
Ngoja tupate majibu ya baadhi ya wagonjwa walokunywa kikombe cha babu, baadhi walisema wamepona na baadhi waliyasema haya;
“Bado sijisikii vizuri ila naomba usiandike mambo yangu kwenye magazeti….dawa niliyokunywa ilifanya kazi kwa siku mbili tu na baada ya hapo ugonjwa umeendelea kama kawaida,” alieleza mgonjwa huyo kwa kifupi akiwa katika hospitali hiyo binafsi (jina limehifadhiwa)
“Bado ugonjwa unaniandama ndugu yangu. Sijapata nafuu yoyote na dawa niliyokunywa Loliondo haijanisadia hata kidogo…..nimeona niendelee tu na matibabu ya hospitali kama nilivyokuwa nafanya awali,” alisema mgonjwa anayeishi Mombo mkoa wa Tanga mwenye asili ya uarabu
“Ukweli ni kwamba bado nina virusi baada ya kufanyiwa vipimo katika hospitali ya Selian. Bado virusi vipo. Nilikuwa nataka kurudi Loliondo nikanywe dawa kwa mara ya pili lakini nimeambiwa tiba ya Babu ni mara moja na hairudiwi tena,” alisema mgonjwa wa ukimwi (jina linahifadhiwa) (Gazeti la Raia Mwema 22-03-2011)
Sasa ngoja tujue nini kilichotokea baada ya viongozi wa dini wa KKKT na wengineo walichokifanya juu ya uendeshwaji na utolewaji wa tiba hii ya kikombe ya Mchungaji Mstaafu:
NI Agosti 25 mwaka 1989 katika ukumbi wa mikutano wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ulioko Oldonyosambu wilayani Arumeru ambako wachungaji 103 wa Kanisa hilo wamekutana wakimsubiri Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini na Kati, Thomas Laizer.
Walikuwa wanakutana kumchagua Mchungaji atakaye kwenda kuziba pengo lililoachwa wazi na Mchungaji Simeone Kiserian wa usharika wa Sonjo mtaa wa Samunge ambaye alikuwa amefariki dunia.Wengi walitarajia suala hilo lingekuwa moja ya ajenda ngumu kutokana na watumishi wengi kutopendelea kwenda eneo hilo kufanya kazi ya kueneza injili kutokana na mazingira magumu ya kazi yaliyopo katika wilaya hiyo ya Ngorongoro.
Mchungaji aliyekubali kwenda kufanya kazi ya kueneza neno la Bwana hakuwa mwingine zaidi ya Mchungaji Ambilikile Mwasapile ambaye alijitokeza kwa hiari yake mwenyewe kuwa alikuwa tayari kwenda eneo hilo kufanya kazi na kuziba pengo lililoachwa wazi.
Ni Mchungaji huyo ambaye sasa ana miaka 78 na akiwa tayari amestaafu kazi tangu mwaka 2002 ndiye amekuwa gumzo kubwa nchini kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa kutokana na madai kuwa amegundua dawa ya ajabu ambayo imekuwa inatibu maradhi sugu kama ukimwi, kansa, kisukari, pumu, shinikizo la damu na mengineyo.
Thomas Laizer na Maaskofu wenzake wawili wa Kanisa hilo na wajumbe wa watu 21 walikwenda Samunge kujionea tiba hiyo na baada ya kuridhika kuwa inatolewa kwa kufuata taratibu za Kikristo walikunywa dawa ya Mchungaji huyo na tayari wanajisikia nafuu baada ya kuinywa. Babu wa Liliondo ni kama vile Padri Nkwera, anafanya kazi ambayo kanisa na Serikali wameshindwa kufanya au hawana uwezo kuwafikia wagonjwa wote. (Gazeti la Raia Mwema 22-03-2011)
Kama hiyo haitoshi, Mchungaji Mwaisapile arudishwa kazini. Wakati Babu Mwasapile akizidi kuvuta watu, Kanisa lake la KKKT limemrudisha kazini kwa kumwongezea mkataba wa ajira usiyo na kikomo, ikiwa ni miaka minne baada ya kustaafu, hivyo kumwezesha kuendelea kupata mshahara na stahili zingine.
Ajira hiyo isiyo rasmi imetokea kwa mchungaji huyo mara baada ya kudaiwa kupata karama kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuanza kutibu magonjwa sugu yakiwemo kisukari, saratani na UKIMWI kwa kile kinachoelezwa kuwa tiba hiyo inafanyika kwa njia ya imani na kimaombi.
Kuajiriwa upya kwa mchungaji huyo kutamwezesha kupata mshahara kama kawaida na kusitisha pensheni aliyokuwa akiipata kama mchungaji mstaafu.
Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini na Kati, Thomas Laiser alithibitisha kurudi kazini rasmi kwa mchungaji huyo jana, akisema kanisa hilo limetafakari na kubaini umuhimu wa mchungaji huyo katika dayosisi hiyo na taifa kwa ujumla, na kumrudisha ili atumikie umma akiwa ndani ya kanisa hilo.
Alisema mchungaji huyo alipewa kazi hiyo na Mwenyezi Mungu tena kazi kubwa kuliko hata ile aliyokuwa akiifanya kabla ya kustaafu, hivyo iwapo ametukuzwa na Mungu kiasi hicho vipi wao wasimjali na kumweka katika himaya ya kanisa.
Mchungaji Mwaisapile ambaye atabakia katika Usharika cha Sonjo alipokuwa akitumikia awali, alistaafu baada ya kulitumikia kanisa hilo katika maeneo mbalimbali, ukiwamo Ushariki wa Babati Mjini, Mkoa wa Manyara kwa miaka saba kabla ya kuhamia Sonjo alikotumikia kwa miaka 12 hadi kustaafu. (Gazeti la Majira 22-03-2011)
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Moravian Tanzania, Alinikisa Cheyo amewaonya viongozi wa dini wanaojiita mabingwa wa uponyaji wanaoponda matibabu ya mchungaji Ambilikile Mwasapile wa Kijiji cha Samunge, Loliondo wilayani Ngorongoro na kuwataka kuacha tabia ya kukaa kwenye maombi ili Mungu awajibu. Alisema “nawambia ndugu zangu katika siku za sasa watu wamekuwa wakiamini sana habari ya Loliondo na kila leo kumekuwa na taarifa za Loliondo, mimi nasema kuwa kinachoponya ni imani ya mtu anayekwenda huko na bila imani atakuwa amepoteza muda kwani mchungaji Mwasapile anamtegemea Mungu”.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Thomas Laiser amewataka wanaochonga juu ya tiba hiyo wafunge midomo yao badala ya kuzuia watu wasikimbilie huko. “Tunachoamini tiba hiyo ina mahusiano makubwa na imani na maombi, na katika maombi kuna kukubaliwa mapema, baadaye na maombi mengine kukataliwa kabisa. Mambo ya Kimungu ni ya Mungu ni vigumu kuyabadilisha kibinadamu, nimekuwa nikipata simu nyingi toka Rwanda, Uganda, Burudi na kwingineko kuom ba mchungaji Mwasapile kubadilisha kituo cha huduma, nawajibu kuwa haiwezekani kwani ni suala la kiimani na maombi hata mchungaji mwenyewe alipenda kutoa tiba hiyo Babati mkoani Manyara alikataliwa”alisisitiza Askofu Laiser. Askofu Thomas Laiser aliendelea kusisitiza kuwa kanisa hilo katika kuhakikisha azma yao inatimia linatarajia kutumia zaidi ya sh milioni 75 katika kuboresha mazingira ya tiba hiyo.
Huduma ya uponyaji inayoendeshwa na Babu imeendelea kuwachanganya baadhi ya viongozi wa dini, wa karibuni kabisa akiwa Mchungaji Christopher Mtikila ambaye ameiponda na kuwaponda waotumia dawa hiyo kutibu maradhi mbalimbali. Licha ya Mchungaji Mtikila kukiri mbele ya waandishi wa habari kuwa dawa hiyo inaponya, ameiponda na kudai kuwa hakuna jipya linaloendelea huko Loliondo. Mchungaji Mtikila jana alitoa mpya pale aliposema 'hata vikombe vinavyotolewa kunywea dawa hiyo ni vya rangi ya kijani na njano, hivyo akadai kwamba hiyo ni zindiko la CCM'. Pia alisema kwamba Loliondo hakuna neno la Mungu, bali ni 'machemsho ambayo wananyeshwa watu bila imani katika Kristo'.
Kiongozi wa Full Gospel Bible Fellowship Askofu Zachary Kakobe wamekuwa wakitoa kauli mbalimbali za kupinga huduma hiyo inayokimbilia na maelfu ya watu wa ndani na nje ya nchi. Askofu Kakobe alivitaja vigezo vya kwenye Biblia takatifu vinavyoonyesha kuwa dawa hiyo si lolote. Kimojawapo kikiwa ni kwamba hakuna huduma ya Mungu ambayo hupangiwa bei! (Gazeti la Majira 21-03-2011)
KHALID: Mbona kanisa linamsimamia kidete Babu wa Loliondo na kuapa kuwa sambamba naye kwa hali na mali? Hii ni wazi kuwa suala la Babu ni la kidini, waislamu tusiwe wajinga wa kumkubali/kuikubali tiba yake kwa njia yoyote ile.
Kuwepo kwa sura kisiasa kulijitokeza wiki mbili zilizopita ambapo Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isidore Shirima kumzuia Mchungaji huyo kuendelea na tiba yake, lakini siku moja baadaye Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), Wiliam Lukuvi alitengua amri hiyo na kuagiza utoaji tiba uendelee kwa hoja kwamba suala hilo lilikuwa la kiimani zaidi.
KHALID: Ona viongozi ambao tumewapa madaraka ya kutuongoza wanavyoshabikia suala lisilo na mantiki na la kipumbavu. Hivi kiongozi kama huyu anaweza akaleta mabadiliko ya kweli kwenye jamii kama kuondoa ufisadi na rushwa? WAISLAMU TUWE MAKINI TUCHAGUAPO VIONGOZI.
Makamishna waandamizi na makamanda kadhaa wa Jeshi la Polisi nchini walitinga kwa babu kupata kikombe hicho.Viongozi hao wa jeshi hilo walipata fursa hiyo baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa watendaji wa jeshi hilo uliofanyika Chuo cha Polisi Moshi hivyo wakaona watumie furasa hiyo kumfikia Babu kabla hawajarudi katika vituo vyao vya kazi. (22-03-11—majira)
KHALID: Hawa nao ni wana usalama katika jamii, Hivi wananchi tutakuwa salama kweli wakati tulowaweka kutulinda hawana usalama, hawafikiri na kuchunguza kabla ya kutenda? Kwa hakika wananchi hatuna budi tuchukue tahadhari za haraka juu ya viongozi wetu ama si hivyo tutaingizwa gizani(kwenye upotevu ulio mkubwa).
Ya Loliondo yanadhihirisha jinsi Watanzania tusivyopenda kuhangaisha akili zetu kufikiri. Sisi tu wavivu wa kufikiri, na wavivu wa kuchanganua mambo. Tumezoea njia za mkato hata kwenye masuala nyeti kama ya tiba. Na Babu wa Loliondo amekuwa njia ya mkato kwa wagonjwa wengi! Tafakari.
Nayo Serikali haikushighulisha kichwa ktk suala la loliondo, Mchungaji mstaafu wa KKKT, Ambilikile (Babu) alisema hadharani wala hakusema kwa siri kuwa dawa yake imepata uponyaji wa kimungu.Ni neno la Mungu ndilo linatibu. Tena akaeleza kuwa dawa yenyewe ameoteshwa katika ndoto na Mungu, hivyo akakiri kuwa dawa yake ni tofauti na dawa nyingine kwani dawa nyingine mgunduzi ni mwanadamu na zimefanyiwa utafiti, lakini hii ya Loliondo ni ya neno la Mungu lililomjia katika ndoto.
Tunukuu kauli ya serikali na wataalamu wake, “Serikali imesema imeridhishwa na dawa inayotolewa na Mchungaji Ambilikile Mwasapile wa Kijiji cha Samunge, Loliondo ikisema haina madhara yoyote kwa matumizi ya binadamu. Akitoa tamko la timu ya wanasayansi waliofanya uchunguzi wa awali wa tiba hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Charys Ugullum, alisema timu hiyo ilianza utafiti wake wa awali Machi 7, mwaka huu. Alisema timu hiyo ilijumuisha wataalamu kutoka Wizara ya Afya, TFDA, Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Mkemia Mkuu wa Serikali na Taasisi ya Utafiti wa Dawa za Asili ya Chuo Kikuu cha Afya ya Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Katika suala hili kwanza serikali imechelewa kutoa tamko, kama dawa hiyo ingekuwa na madhara kwa wanadamu wangapi wangeathirka, na kwanini serikali ilisubiri muda mrefu wote mpaka karibu viongozi wote wa serikali wamekunywa ndipo inatoa tamko. Ni uzembe au kutokuwa makini?
Hivi wasomi hawa wote hawakufikiri hata mara moja kuwa ni ujinga kupima kitu kilichosemwa ni neno la Mungu kwa kutumia vifaa vya maabara?. Tangu lini na wapi ndoto zinapimwa kwa kutumia vifaa vya maabara, Mkemia Mkuu anajua nini kuhusu Elimu ya ndoto?. Dawa inayosemekana inatoka kwa Mungu, inayolingana dozi kwa kila ugonjwa, inayohusisha imani kabisa bila nguvu za kisayansi, kweli serikali ilipaswa kutenga pesa kutafiti kama neno la Mungu linatibu? Serikali yenyewe ingemwona wapi Mungu na kuuliza nguvu ya uponyaji ya huo mti uliokuwepo katika mazingira hayo kila siku?
Serikali bila aibu inasema, “tena kinachofuata sasa tutachunguza kama kweli dawa hiyo inatibu magonjwa hayo matano aliyoyasema Babu. Hivyo wananchi wawe na subira ili watupe nafasi tufanye utafiti wa kina zaidi.” Je, ikitokea kuwa dawa hiyo haitibu watachukua hatua gani?
Mkurugenzi wa Uendelezaji na Uratibu Utafiti kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia, Dk. Rose Kingamkono akasema wanafuatilia ili waweze kujua kama kuna hatimiliki ya tiba hiyo. Aliendelea kusema “Wananchi wasitoe mbegu au mti huo ovyoovyo maana wajanja wanaweza wakauchukua kwenda kutengeneza dawa kisha kuja kutuuzia tena kwa gharama kubwa.” Jamani viongozi wa serikali yetu wanafikiri sawa sawa? Mti upo porini, inasemekana umetiwa nguvu ya uponyaji na Mungu kwa kupitia mchungaji Mwasapile, wala si mtu mwingine, ndiyo maana hata wataaalamu hao wa tiba hadi sasa hawajachukua mizizi kupeleka Muhimbili, Bugando au KCMC kutibu wagonjwa, iweje mtu afikirie neno la Mungu kuwekewa hatimiliki, na kuzuia nguvu ya utendaji au uponyaji wa Kimungu usiende kwingine? Je, mtu mwingine akiota Kenya leo, Uganda kesho na Uturuki wiki ijayo na kupewa uwezo kama wa Mwasapile, serikali yetu itazuia huduma za ndoto za Kimungu katika mataifa mengine kwa kuwa mtanzania ndio alikuwa wa kwanza kuota ndoto na kupewa maelekezo na Mungu?
Msajili wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Dk. Paulo Mhame alisema hivi sasa wako katika hatua za mwisho za kumpatia cheti cha usajili Mchungaji Mwasapile. Wanampatia kama mganga wa jadi kwa utaratibu upi?
NDUGU ZANGU TUCHUKUE TAHADHARI JUU YA VIONGOZI WETU, WANATUDHALILISHA KWA MAMBO WANAYOYAFANYA, MBONA HAWASHUGHULISHI VICHWA VYAO. VIONGOZI WENYEWE WANAOHIMIZA KUWEPO KWA TIBA HII WOTE NI WAKRISTO HIVYO TUJUWE WAZI KUWA HAPA KUNA UDINI, PIA WANATETEANA ILI KUUENDELEZA UDINI WAO. WAISLAMU TUWAMKE TUGOMBEE KWA WINGI NAFASI ZA UONGOZI AMA SIVYO TUTARITADISHWA.
Namnkuu Paroko mmoja aliyetupa mawazo ya kujifikirisha kidogo kuwa "Sina chuki wala tatizo lolote na tiba ya Loliondo, lakini kama unataka kwenda lazima ujiulize maswali manne yafuatayo:
Kwanza, tiba inayotokana na miujiza ya Mungu lazima iwe endelevu, isiwepo kwa kipindi kifupi tu.
Pili, watu wajiulize kama miujiza kutoka kwa Mungu huwa na masharti?
Tatu, wajiulize kama tiba hiyo inafanya kazi ndani ya Loliondo, kwanini isifanye kazi Dar es Salaam na kwingineko?
Nne, wajiulize kuhusu tiba hiyo ya magonjwa sugu ukiwemo ukimwi, je, Mungu aliwaumba wanadamu na kisha kuamua kuwaangamiza? Au wanadamu wanaangamia kutokana na vitendo vyao vya ujanja ujanja?” (Gazeti la Tanzania daima 30-03-2011)
Hao ndo yale yalojiri kutokana na tiba ya Mchungaji Mstaafu Ambilikile Mwasapile maarufu kwa jina la ‘Babu’ wa Loliondo. Nao wengine wajitokeza kutoa huduma ya tiba ya kikombe katika sehemu mbalimbali nchini Tanzania, pata hii;
TIBA YA KIKOMBE ROMBO
KUTOKANA na kujitokeza kwa mtu mwingine wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro anayetoa dawa ya kutibu magonjwa sugu kama alivyo Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwaisapile 'Babu', mtu huyo amesitishwa na Ofisa Mtendaji wa Kata kuendelea na huduma hiyo.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu, kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Hilali James, umri (28), alisema endapo Serikali itashikilia msimamo wake wa kuendelea kuisitisha huduma yake, tayari ameoteshwa ndoto kuwa atatokea mtu mwingine ambaye ataendelea kuitoa huduma hiyo.
James alisema huduma hiyo alikuwa akiitoa katika Kijiji cha Mbomani Chini Kata ya Tarakea wilayani Rombo, ambapo masharti yake ni mtu kutakiwa kunywa vikombe viwili kwa wakati mmoja na hairuhusiwi kurudia.
Mbali na kunywa, alisema alioteshwa ndoto kuwa atapokea Sh 500/=, ambazo kati ya hizo, Sh 200/= ni kwa ajili ya matumizi yake ya kuwalipa wafanyakazi, na Sh 300/= za kuwasaidia yatima na watu wasiojiweza. Akizungumzia magonjwa yanayotibiwa na dawa yake, alidai inatibu shinikizo la damu, kisukari pumu, saratani, figo, Ukimwi na magonjwa ya tumbo. Pia alidai tayari watu wapatao 100 wamekwisha inywa dawa hiyo na kupata uponyaji.
Kijana huyo mwenye mke na watoto wanne, alibainisha kuwa awali alikuwa fundi wa baiskeli, na kwamba chanzo cha kuanza kutoa dawa hiyo ni kutokana na kuoteshwa ndoto na Yesu Kristo usiku na mchana. Alisema mti aliooteshwa kuutumia hadi sasa hajaufahamu jina lake, na kuwa ulikuja katika ndoto na hajawahi kuuona tangu kuzaliwa kwake.
Alisema yeye kuibuka baada ya Mchungaji Mwaisapile si tatizo kwa sababu, kila jambo lina wakati wake, hivyo wakati huu ni wake. (21-03-11 Habari Leo)
KHALID: Ndugu zangu waislamu tufumbuke macho. Mbona hizi tiba zote asili yake ni ndoto tu hamna hata maandiko!? Mbona tunataka tubabaishwe na watu wanaoota?! Hivi wangapi mpaka leo wanaota, je wakiamua kutangaza ndoto waotazo itakuaje? Ndugu yangu umizwa kichwa katika kila tukio litokealo ili kujua undani wa tukio hilo na si kukurupuka na kuchukua maamuzi yasiyo na msingi.
TIBA YA KIKOMBE MBEYA
SERIKALI Mkoa wa Mbeya jana ilisalimu amri kwa mganga aliyeibuka akitibu magonjwa mbalimbali, Jafari Welino, umri (17) na kujikuta ikibariki huduma baada ya wagonjwa wanaotegemea huduma hiyo kuandamana na kutishia kulipua Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Akijibu maswali kijana huyo aliyeonekana mwenye ujasiri alisema kuwa yeye alipewa kazi hiyo baada ya kutokewa na mzimu (wa mama yake mzazi) katika usingizi/ndoto ambapo alikatazwa kusoma shule na kuoneshwa mti ambao aliambiwa kuwa utakuwa ukombozi kwa watu kwa kuwapa vikombe viwili kwa siku mbili bila ya malipo.
Taarifa ya awali iliyolifikia gazeti la majira la tarehe 29-03-2011 (soma uk. 9) ilisema kuwa Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ilikuwa imemzuia kijana huyo kutoa huduma ya tiba kwa madai kuwa mazingira ya utoaji wa huduma hiyo ni machafu na kuwa dawa anayotumia ilitakiwa ifanyiwe uchunguzi ili kuona kama ni kweli inaweza kuponya magonjwa sugu bila kuleta madhara kwa afya za binadamu.
Kutokana na hali hiyo, baada ya wagonjwa waliokuwa wamefika nyumbani kwa kijana huyo eneo la Mabatini, kilomita 2.5 kutoka katikati ya Jiji la Mbeya wakiwa na vikombe mikononi walikubalina kuandamana kwenda kwa mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. John Mwakipesile alitoa amri kwa kijana huyo kuendelea kutoa huduma huku idara zinazohusika zikifuatilia kuona namna ambayo itafanya, ili kijana huyo aweze kutoa huduma katika hali ya usafi wakati utafiti wa dawa hizo ukiendelea.Katibu Tawala Msaidizi Bw. Chitama alisema kuwa serikali haina ugomvi na waganga wala imani za dini, na hivyo kinachotakiwa kwa kijana huyo ni kuhakikisha anafanya kazi hizo katika mazingira safi ili kutoathiri afya za wagonjwa wake.
Kuhusu kuhama katika eneo hilo, alisema kuwa hawezi kufanya hivyo kwa agizo la serikali badala yake anasubiri mizimu yake iweze kumweleza jambo hilo na sehemu ya kwenda na ndipo atakapoamua kufanya hivyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Bw. Advocate Nyombi alisema yeye anachoangalia ni hali ya usalama wa watu wanaomiminika katika eno hilo dogo kupata huduma, huku akitaka mamlaka nyingine zifanye kazi yake ili kudhibiti uvunjifu wa amani unaoweza kutokea. (Gazeti la Majira 29-03-2011)
KHALID: Sasa basi inatosha, mnataka mpaka mizimu nayo tuiamini? Hakika hii ni shirki kubwa tena ilo wazi kabisa na atakayemshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote atakuwa amepotea upotevu ulo mkubwa kabisa. Hivi kwa nini hawa viongozi wetu wa nchi wenye dini isiyokuwa ya kiislamu wanazikubali tiba hizi? Bila shaka si bure ndugu zangu wa kiislamu WANATAKA TUFUATE MILA ISIYOKUWA YA KIISLAMU.
TIBA YA KIKOMBE TABORA
Tiba hii inatolewa na Magreeth mutalemwa, umri miaka (40) mkazi wa Tabora, alianza kutoa huduma hiyo tangu tarehe 21-03-2011. Pia alisema “Nilikuwa nikipata msukumo baada ya kuoteshwa kabla ya tarehe 21 na kuidharau ndoto ile nilianza kupata matatizo lakini baada ya kuanza kufanya yale niliyotakiwa kufanya matatizo yakaisha ndio mpaka leo natibu watu”
Pia aliwazungumzi wenzake ambao wanatoa tiba kama yake kwa kusema yafuatayo “Ah ninavyoona mimi huu ni uwezo wa Mwenyezi Mungu tu, kwani katika uoteshwaji wangu nakumbuka sauti iliniambia tupo watatu na tumetunukiwa roho safi kufanya shughuli hii ya kutoa tiba. Kwa hiyo naamini hao ni wawili na mimi ni wa tatu na ndio tuliotunukiwa”. (keronyingi.blogspot.com tarehe 29-03-2011)
Waandishi wa Dar Leo walishuhudia viongozi wa vituo vikuu vya afya wakifika katika eneo analotoa dawa mwanamke huyo na kuchukua sampuli ya dawa hiyo.Wakati hayo yakiendelea mwanamke huyo Magreth Mutalemwa ambaye anatoa dawa hiyo kwa njia ya maombi kwanza amesema kuwa, anasikitishwa na baadhi ya wajanja ambao wamekuwa wakifika kwa nia ya kumjaribu kwa njia ya ushirikina.
Amesema kuwa, amekuwa akipata majaribu mara kwa mara tangu aanze kutoa tiba hiyo lakini kwakuwa anatumia zaidi imani ya kidini wachawi hao wamekuwa wakishindwa kutekeleza azma yao.Hata hivyo wakati wizara hiyo ikitoa tamko hilo mamia ya wakazi wa mkoa huo pamoja na vitongoji vya jirani wamekuwa wakiendelea kufurika kupata tiba kwa mwanamke huyo.Kutokana na hali hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Liberatus Barlow amemwaga askari wa mkoa huo katika eneo hilo ili kuimarisha ulinzi. (Gazeti la Dar Leo 31-03-2011)
KHALID: Ndugu zangu katika imani, hapa hamna tiba bali ni Uchawi, Ushirikina, Utapeli/Ulaghai na Udini ndo unatawala. WAISLAMU TUSIKUBALI KUBABAISHWA NA YOYOTE YULE.
Haya ndo yale yalojiri katika tiba hii ya kikombe mpaka leo tarehe 02-04-2011nimeandika, ambayo inatibu aina zote za magonjwa sugu uzijuazo, lakini nikiwa kama muislamu, inanilazimu mimi na wewe uliyesoma makala hii KUKUTAHADHARISHA NA KUMTAHADHARISHA NDUGUYO MUISLAMU JUU YA TIBA HII YENYE SHIRKI NDANI YAKE. Katika mafundisho ya kiislamu tumefundishwa yafuatayo;-
Hadithi ya Mtume (S.A.W), Kutoka Abu Huraira(R.A) Hakika Mtume (S.A.W) amesema “Yoyote atakayemuendea mpiga ramli / kuhani(ambaye mashetani wamemfundisha) akamuuliza jambo na akamsadikisha kwa yale aloambiwa na kuhani basi atakuwa amekufuru/amekanusha yale alokuja nayo Mtume (S.A.W)” Imepokelewa na watu wa Sunnah na Hakim
Kutoka kwa baadhi ya wake za Mtume(S.A.W) kutoka kwa Mtume (S.A.W) amesema “Atakayemuendea Mpiga ramli na akmuuliza juu ya jambo, haitokubaliwa sala yako siku arobaini” Sahih Muslim
Kama ukifuatilia kwa undani utagundua kuwa hamna tiba yoyote ni uzushi, uongo na ni propaganda za wasiokuwa waislamu kutaka kuwatawala watu kifikra. Allah (S.W) anasema katika Qur’an tukufu:-
“Hiki ni Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake; ni uwongofu kwa wachamungu”.(Qur’an 02:02)
“Wala msiseme uwongo, kwa kuropokwa na ndimi zenu: Hichi halali, na hichi haramu - mkimzulia uwongo Mwenyezi Mungu. Hakika wanao mzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawatafanikiwa”
(Qur 16:116)
“Enyi mlio amini! Akikujieni mpotovu na khabari yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kutojua, na mkawa tena wenye kujuta kwa mliyoyatenda” (Qur’an 49:06)
Kwa maana “Enyi mlioamini! Akikujieni mtu ambaye yuko nje ya sharia ya Mwenyezi Mungu akakupeni khabari yoyote, basi chungueni mjue ukweli wake, kwa kuchelea msije mkawaletea watu madhara, kwa kutojua hali yao. Hapo tena baada ya kwisha dhihiri kuwa hawana makosa mkaingia katika majuto ya daima, mkatamani yasingeli kuwa.”
“Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao. Na Mwenyezi Mungu atakamilisha nuru yake ijapo kuwa makafiri watachukia(8). Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya haki ili ipate kuzishinda dini zote, ijapo kuwa washirikina watachukia(9)”. (Qur’an 61:08-09)
“Wala msichanganye kweli na uwongo na mkaificha kweli nanyi mnajua.” (Qur’an 02:42)
Kwa maana kuwa “Wala msichanganye Haki iliyo toka kwangu na upotovu mlio uzua nyinyi, hata ikawa halijuulikani la kweli na la uwongo. Wala msiifiche Haki, na katika hiyo Haki ni kumsadiki Muhammad, na nyinyi mnajua kuwa yeye ni wa kweli na wa kusadikiwa”
“Enyi mlio amini! Msiwafanye wasiri wenu watu wasio kuwa katika nyinyi. Hawataacha kukufanyieni ubaya. Wanayapenda yanayo kudhuruni. Imekwisha fichuka chuki yao katika midomo yao. Na yanayo ficha vifua vyao ni makubwa zaidi. Tumekwisha kubainishieni Ishara ikiwa nyinyi mtayatia akilini”
(Qur’an 03:118)
“Mayahudi hawawi radhi nawe, wala Wakristo, mpaka ufuate mila yao. Sema: Hakika uwongofu wa Mwenyezi Mungu ndio uwongofu. Na kama ukifuata matamanio yao baada ya ujuzi ulio kwisha kujia, hutapata mlinzi wala msaidizi kwa Mwenyezi Mungu” (Qur’an 02:120)
“Mwenyezi Mungu, na Malaika, na wenye ilimu, wameshuhudia kuwa hakika hapana mungu ila Yeye, ndiye Mwenye kusimamisha uadilifu; hapana mungu ila Yeye Mwenye nguvu na Mwenye hikima(18). Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Na walio pewa Kitabu hawakukhitalifiana ila baada ya kuwajia ujuzi, kwa sababu ya uhasidi ulio kuwa baina yao. Na anaye zikataa Ishara za Mwenyezi Mungu basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu(19).” (Qur’an 03:18-19)
“Hakika wanaouza ahadi ya Mwenyezi Mungu na viapo vyao thamani ndogo, hao hawatakuwa na sehemu ya kheri yoyote katika Akhera, wala Mwenyezi Mungu hatasema nao wala hatawatazama Siku ya Kiyama, wala hatawatakasa, nao watapata adhabu chungu(77). Na wapo baadhi yao wanao pindua ndimi zao katika kusoma Kitabu ili mdhanie kuwa hayo yanatoka Kitabuni, na wala hayatoki Kitabuni. Na husema: Haya yametoka kwa Mwenyezi Mungu. Na wala hayatoki kwa Mwenyezi Mungu. Na wanamsingizia Mwenyezi Mungu uwongo na wao wanajua(78).” (Qur’an 03:77-78)
“Hakika wale walio kufuru baada ya kuamini kwao, kisha wakazidi kukufuru, toba yao haitakubaliwa, na hao ndio walio potea(90). Hakika wale waliokufuru, na wakafa hali ni makafiri haitakubaliwa kutoka kwa yeyote wao fidia ya dhahabu ya kujaza dunia nzima lau wangeliitoa. Hao watapata adhabu chungu, wala hawatakuwa na wa kuwanusuru(91)”. (Qur’an 03:90-91)
“Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu(102). Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka(103)” (Qur’an 03:102-103)
“Enyi mlioamini! Ikiwa mtawat'ii waliokufuru watakurudisheni nyuma, na hapo mtageuka kuwa wenye kukhasiri(149). Bali Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wenu, naye ndiye bora wa wasaidizi(150).” (Qur’an 03:149-150)
“Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kushirikishwa, na husamehe yaliyo duni ya hilo kwa amtakaye. Na anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu basi hakika amezua dhambi kubwa” (Qur’an 04:48)
Pia Muislamu kuwa makini kwa kila tukio linalotokea dunia na hasa yale ambayo yanatokea kwa wasiokuwa waislamu kwani Allah(S.W) anatuhaikishia ktk Qur’an kuwa wasiokuwa waislamu hawana mapenzi/urafiki/nia njema na waislamu, lengo lao ni kuwabadilisha waislam na kuwafanya wafuate mila za wasiokuwa waislamu.
Allah(S.W) ndo mjuzi zaidi.
MUISLAMU CHUKUA TAHADHARI KWA KUTOISADIKISHA TIBA HII
NB: Kuwa makini pindi usomapo kwenye maneno yalopigiwa mstari
ALLAH SHUHUDIA KUWA NIMEFIKISHA
HAKUNA MKAMILIFU ISIPOKUWA ALLAH (S.W)
Kwa ushauri, msaada, changamoto, mapendekezo, nyongeza katika kuupeleka mbele uislamu, tuwasiliane kwa 0713174345, 0762121619, khalidbilaly@bismillah.com, khalidbilaly@yahoo.com.
WABILLAHI TAWFIIQ
ALLAH HELP US
TUWEKE MAZINGATIO
13 years ago
No comments:
Post a Comment