بسم الله الرحمن الرحيم

kutafuta elimu ni faradhi kwa kila muislamu
الحمد لله الذي نستعينه ونستغفره ونعوذ بالله من شرور أنفسنا ومن سيئات أعمالنا من يهد الله فلا مضل له ومن يضلل فلا هادي له .



ونشهد أن لا إله إلا الله وحده لا شريك له ونشهد أن محمدا عبده ورسوله أرسله بالهدى ودين الحق ليظهره على الدين كله وكفى بالله شهيدا




Wednesday, April 27, 2011

MWANAMKE WA KIISLAMU: HADHI YAKE KATIKA UMMAH
Shaykh 'Abdul-'Aziyz Ibn Baaz (RahimahuLlaah)
Siri ya umuhimu wa mwanamke wa Kiislam inatanda katika mzigo mkubwa na jukumu ambao alilowekewa mbele yake, na mashaka ambayo yako katika mabega yake. Jukumu na mashaka ambayo hata mengine mwanamme anaweza kubeba.
Hadhi ya mwanamke katika Uislam ina cheo kikubwa na iliyo na taadhimu, na taathira yake ni kubwa mno katika maisha ya kila Muislamu. Kwa kweli mwanamke wa Kiislamu ni mwalimu wa kwanza katika kujenga jamii njema, ikiwa kama atafuata mwongozo kutoka katika Kitabu cha Allaah na Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa sallam).
Mtume Muhammad (Swalla Allaahu alayhi wa sallam) amesema: "Nakuachieni vitu viwili, hamtapotea kamwe kama mkivishikilia kwa nguvu vyote viwili hivi, Kitabu cha Allaah na Sunnah zangu.
Kama ilivyokuwa katika ukawaida wa Qur-aan na Sunnah humwekwa kila Muislamu mwanaume au mwanamke mbali na upotofu kwa njia yeyote. Upotofu ambao mataifa mbali mbali yanaugua, na upotofu wao hauji ila kwa sababu ya kuwa mbali kabisa na njia ya Allaah, ambaye ni Mkamilifu kushinda wote, Aliye juu kabisa, na pia kuwa mbali na yale ambayo Mitume na Manabii wake (Rehma na Amani ziwafike juu wao wote) wamekuja nayo. Umuhimu mkubwa wa mwanamke wa Kiislam ikiwa mke, dada, au binti, haki ambazo zinatakiwa kutimizwa kwake na haki ambazo anatakiwa kutimiza zimefafanuliwa katika Qur-aan Tukufu, na maelezo zaidi ya haya yamefafanuliwa katika Sunnah iliyotakasika.
Siri ya umuhimu wake umetanda katika kazi yake nzito na mamlaka ambayo yamewekwa juu yake, na shida ambazo anabeba mabegani kwake - mamlaka na dhiki ambazo hata mwanaume hawezi kuzibeba. Ndio maana imelazimishwa kwa mtu kuonyesha hisani kwa mama yake, kuonyesha upole na uhusiano wa ukaribu ulio mzuri kwake. na katika jambo hili, apewe ubora kuliko baba mtu. Mwenyezi Mungu Mtukufu kasema:
"Na Tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni Kwangu Mimi ndiyo marudio." [Surah Luqmaan 31:14].
Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kasema,
"Na Tumemuusia mwanaadamu awatendee wema wazazi wake wawili. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu. Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini". [Surah Ah'qaaf 41:15].
Mtu alikuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu alayhi wa salam) na akasema,
"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Nani miongoni wa watu wote anastahiki uhusiano wangu wa karibu?" Mtume akajibu. "Mama yako"
Yule mtu akauliza tena, "kisha nani?" Mtume akamjibu
"Mama yako"
Yule mtu akauliza tena, "kisha nani?" Mtume akamjibu
"Mama yako"
Yule mtu akauliza tena, "kisha nani?" Mtume akamjibu.
"Baba yako"
Kwahiyo haya yanasisitiza kwamba mama mtu anapewa heshima mara tatu kuliko baba mtu.
Na kuhusu mke, hadhi yake na taathira yake katika kutuliza moyo na kuliwaza imeonyeshwa wazi wazi katika Aayah Tukufu (kauli ya Allaah), katika msemo wake Mtukufu,
"Na katika Ishara Zake ni kuwa Amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye Amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri. [Suuratur-Ruum 30:21].
Al-Haafidh Ibn Kathiyr (Aliyefariki 774H) - RahimahuLLaah - alisema katika kufafanua neno ‘Mawaddah’ na ‘Rahmah’ ambayo inapatikana katika Ayaah iliyopita, anasema:
"Al-Mawaddah inamaanisha mapenzi na mahaba na Ar-Rahmah inamaniisha rehma (upole) na huruma - kama ilivyokuwa mtu anamchukuwa mwanamke ama kwa sababu ya mapenzi kwake, au kwa sababu ya mapenzi juu yake au kwa sababu ya upole na huruma juu yake, kwa kumpa mtoto kutokana na yeye..."
Na jinsi mke wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Bi Khadiyjah (Radhiya Allaahu 'anha) alivyosimama kwa namna ya pekee kusaidia sana kumliwaza na kumtuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) wakati Jibriyl ('alayhis-salaam) alipojitokeza kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kwa mara ya kwanza katika pango la Hiraa. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alirudi kwa Bi Khadiyjah (Radhiya Allaahu 'anha) akiwa na wahyi wa kwanza na huku moyo wake unapiga na kutetemeka kwa nguvu, na akamwambia Bi Khadiyjah:
"Nifunika! Nifunike!"
Kwa hiyo, (Bi Khadijah) akamfunika mpaka hofu yake ilipotokomea, baadaye Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akamuelezea Bi Khadiyjah (Radhiya Allaahu 'anha) kila kitu kilichotokea na akasema
"Naogopa juu ya kutokewa na kitu kibaya"
(Bi Khadiyjah) akamwambia,
"Abadan! WaLlaahi! Allaah hatokuangusha. Unaweka mahusiano mema baina yako na jamaa zako, unawasaidia masikini na fukara, unawahudumia wageni wako kwa ukarimu na unawasaidia wale ambao wamekumbwa na maafa.".
Na usisahau kuhusu mama wa waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) pamoja na taathira yake. Hata Maswahaba watukufu walikuwa wanajipatia elimu ya Hadiyth kutoka kwake., na wengi katika Maswahabiyaat (wafuasi wa kike wa Rasuulu-Allaah) walijifunza vitu mbali mbali kuhusu Sharia zilizowahusu wanawake kutoka kwake.
Sina shaka ya kwamba mama yangu- Allaah Amrehemu - alikuwa na taathira makubwa juu yangu, alikuwa ananihimiza nisome, na alikuwa ananisaidia kwa hilo. Allaah Amuongezee thawabu na Amlipe kwa malipo mema kwa yote aliyonifanyia.
Na pia bila shaka, nyumba ambayo ina huruma, upole, upendo na kujali, pamoja na mafundisho mema ya Kiislam itamuathiri mtu. Kwa hiyo atakuwa - ikiwa Allaah atapenda - mwenye kufanikiwa katika mambo yake na katika kitu chochote - ikiwa kutafuta ilmu, biashara, kupata maisha mazuri, au vingine baada ya hivi. Kwahiyo ni Allaah peke Yake ninayemuomba Anipe mafanikio na Atuongoze sote kwenye yale ambayo Anayapenda na Anaridhia. Na Salam na Amani za Allaah zimfikie Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) na familia yake, Maswahaba zake na wafuasi wake.

No comments: